Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limevitaka baadhi ya
vyombo vya habari nchini kuacha mara moja kampeni za upotoshaji zenye
lengo la kuwachafua viongozi wa juu wa shirikisho hilo.
TFF imeshtushwa na taarifa inayoendelea kutolewa kwenye gazeti moja
la kila siku ikidai kuwa kuna ufisadi ndani ya shirikisho wakati madai
hayo ni ya uongo na yenye lengo la kujenga mtazamo hasi dhidi ya
shirikisho na viongozi wake.
Gazeti hilo la kila siku limetumia taarifa ya ukaguzi wa fedha
iliyofanywa na wakaguzi kutoka TAC kujenga picha kuwa ni ushahidi tosha
wa kuwepo kwa ufisadi ndani ya shirikisho.
Taarifa ya ukaguzi wa fedha ya TAC haikuwahi kuituhumu TFF kwa
ufisadi. Taarifa ilibaini maeneo ya kiuhasibu ambayo yalihitaji maelezo
ya ziada ya namna baadhi ya malipo yalivyofanyika (audit queries), na
ufafanuzi ulitolewa kwa ufasaha na watendaji wa shirikisho na kupelekwa
mbele ya Mkutano Mkuu wa Shirikisho.
Hata hivyo gazeti hilo ambalo limeonekana kuweka kando kabisa misingi
ya uandishi wa habari, limechapisha taarifa bila hata kutoa nafasi kwa
wanaotuhumiwa kujibu na kutoa ufafanuzi stahiki.
Rais na katibu mkuu wa shirikisho wanahudhuria mikutano ya CAF nje ya
nchi wakati gazeti hilo likiendelea kuporomosha mlolongo wa tuhuma bila
kutoa haki ya kusikilizwa kwa wanaoandikwa vibaya.
TFF inaliangalia suala hili kama kampeini chafu inayofanywa ili
kushawishi matokeo ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Agasti mwaka
huu.
Pia taarifa hii potofu inalenga kulihamisha taifa kutoka kwenye
masuala ya msingi kama kuiunga mkono Serengeti Boys kwenye mashindano ya
Afrika na kuanza kujadili masuala yanayohusiana na siasa za uchaguzi wa
TFF.
TFF kwa sasa inatafakari hatua za kisheria za kuchukua dhidi ya
vyombo vya habari husika na inachukua nafasi hii kuvisihi vyombo vya
habari kuacha mara moja kujihusisha na kampeni ya kuchafuana ambayo ni
kinyume na misingi ya maadili ya uandishi wa habari.
About Author

Advertisement

Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment