Timu ya Taifa ya wasichana
wenye umri wa chini ya miaka 20 (Tanzanite), imewasili salama nchini ikitokea
Nigeria ambako ilicheza mechi ya awali dhidi ya wenyeji Nigeria katika mchezo
wa kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Ufaransa.
Timu hiyo iliwasili saa 9.00 usiku wa kuamkia
Jumanne Septemba 19, 2017 na kulakiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Kidao Wilfred; Bw. Kaimu Mkurugenzi wa
Mashindano, Bw. Jonas Kiwia na Ofisa Habari wa TFF, Bw. Alfred Lucas.
Mara baada ya kurejea, Kocha Mkuu wa timu
hiyo, Sebastian Nkoma, amesema walipoteza mchezo wa awali kwa kufungwa mabao
3-0 kwa sababu Nigeria ni timu bora na Tanzanite kwa sasa wanajipanga kwa ajili
ya mchezo wa marudiano.
“Kwa kuwa tulionesha kiwango bora, ni
matumaini yangu kwamba tutafanya vema kwenye mchezo wa marudiano hapa nyumbani
na tutasonga mbele,” amesema Nkoma ambaye ndoto zake ni kuipeleka Tanzanite
Ufaransa mwakani.
Mchezo wa marudiano utafanyika Oktoba mosi,
mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam, ulioko Chamazi, Dar es Salaam
Wakati timu ikionekana ina ari ya kufanya vema
kwenye mchezo wa marudiano, Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Kidao Wilfred aliwapa shime
kufanya vema kwenye mchezo wa kirafiki na kusisitiza kambi kuendelea mpaka
mchezo wa maruadiano.
Mkuu wa Msafara, Bi. Amina Karuma, alisema
kuwa mapambano bado yanaendelea na anaamini kikosi chake kitashinda katika
mechi ya marudiano itakayochezwa baada ya wiki mbili. Karuma pia ni Mwenyekiti
wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Tanzania (TWFA).
Aliongeza kuwa anashikuru wachezaji wote ni
wazima na wataendelea na kambi ili kujiandaa na mchezo wa marudiano huku
akiahidi kuwatafutia mechi ya kirafiki kabla ya kuwakaribisha Nigeria.

Post a Comment