Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), chini ya Makamu Mwenyekiti, Peter Hellar ilikutana jana
Jumatano Agosti 30, mwaka huu ikiwa na ajenda kuu ya mashauri yanayohusu
wachezaji watatu.
Wachezaji hao ni Obrey Chirwa wa
Young Africans pamoja na wenzake wawili Deus Kaseke na Simon Msuva ambao kwa
pamoja msimu uliopita walikuwa wanaitumikia klabu hiyo ya Jangwani.
Wachezaji hao walisimamishwa
kucheza soka katika uamuzi uliofanywa na Kamati ya 72 ya Bodi ya Ligi kwa
mujibu wa kanuni ya 9 (5) ya Ligi Kuu kutokana na kumvamia na kumsukuma mwamuzi
Ludovic Charles aliyechezesha mechi ya Young Africans na Mbao Mei 20, mwaka
huu.
Kati ya watuhumiwa wote, Kamati
ilimtia hatiani Simon Msuva na kuwaachai huru Deus Kaseke na Obrey Chiwa. Msuva
alionekana kumvamia na kumwangusha mwamuzi kinyume cha kanuni ya 49 (1) (b)
ambako sasa anatakiwa kusimama mechi tatu za aina yo yote ya mashindano ya
ndani.
Kwa mujibu wa Wakili Hellar
tayari Msuva alikosa mechi za mashindano ya Sportpesa hivyo Kamati imetambua
kwamba tayari ametumikia adhabu husika, lakini inampa onyo kali la maandishi
kwa mujibu wa kanuni ya 14.
Kamati imeshauri TFF na Bodi ya
Ligi ni vema kuachia Kamati majukumu ya kusimamisha na kufungia kwa mujibu wa
kanuni za kinidhamu badala ya taasisi hizo kuchukua hatua ya kusimamisha ambazo
hazileti haki na usawa uwa ni kama adhabu.
Ushauri huo umepokelewa na TFF na
itaufanyia kazi.
Itakumbukwa kwamba mechi
iliyowaletea shida wachezaji hao ni namba 236 ya Ligi Kuu ya Vodacom
iliyofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Yanga ikipoteza kwa bao 1-0.
Mara baada ya mchezo huo, Kamati
ya 72 ya Bodi ya Ligi ilipitia matukio mbalimbali na kufikia uamuzi wa
kuwasimamisha wachezaji Deus Kaseke, Simon Msuva na Obrey Chirwa wa Yanga
kucheza mechi za Ligi Kuu.
Walisimamishwa wakisubiri suala
lao la kumsukuma na kumwangusha Mwamuzi Ludovic Charles kusikilizwa na kutolewa
uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Wachezaji hao walidaiwa kufanya
kitendo hicho katika mechi hiyo dhidi ya Mbao FC iliyofanyika Mei 20, 2017
kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijni Mwanza. Uamuzi wa Kamati ya Saa 72
ulizingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu.
Itakumbukwa, Mwamuzi Ludovic
Charles amepewa onyo kali kwa kutodhibiti vizuri mchezo. Uamuzi dhidi yake ni
kwa mujibu w Kanuni ya 38(5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.


Post a Comment