Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Kidao Wilfred ameunda kikosi kazi cha
wataalamu wanne wa shirikisho kuangalia upya ratiba ya Ligi Kuu ili kuondoa
kila aina ya kero inayoweza kuibuka katikati ya mashindano.
Kidao ambaye ana siku tisa
ofisini tangu ashike wadhifa huo, amesema kuna changamoto nyingi sana katika
shirikisho, lakini kubwa ni hili ambalo wanafamilia ya mpira wa miguu wamekuwa
wakijadili kwa sasa.
Wadau wanajadili suala la ratiba
ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Kwamba baada ya michezo ya
mzunguko wa kwanza tu, ratiba imetangazwa kubadilishwa. Ni kweli imebadilishwa
kwa sababu ya kupisha wiki ya kalenda ya FIFA ya mechi ama za ushindani au
kirafiki kati ya nchi na nchi.
Amesema kwamba makosa yamefanywa
na maofisa wa Bodi ya Ligi Kuu ambayo ndiyo yenye dhamana ya kupanga ratiba ya
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL); Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi
Daraja la Pili (SDL).
Maofisa hao ilihali wakijua
kwamba kuna wiki ya kalenda ya FIFA, walidiriki kupanga mechi za Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara.
Sasa tuchukua nafasi hii kuomba
radhi Watanzania hususani wanafamilia ya mpira wa miguu ambao kwa namna moja au
nyingine wameghafirishwa na kupanguliwa ratiba.
“Lakini suala hili haliwezi
kupita hivi hivi bila hatua na kinidhamu kuchukuliwa. Rais wa TFF Bw. Wallace
Karia aliniagiza nimwandikie Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu, Bw. Boniface
Wambura achukue hatua za kinidhamu kwa maofisa wote waliohusika na upangaji huo
wa ratiba ulioingilia ratiba ya kalenda ya wiki ya FIFA,” amesema Kidao.
Hatua hizi za kinidhamu si kwa
kupanga mechi wakati wa Wiki ya FIFA pekee, bali maofisa hao wamehusika kupanga
ratiba ambayo tathmini ya uongozi imeonyesha kwamba si rafiki kwa timu zote 16
zinazoshiriki VPL.
Hii ni kwa sababu kuna baadhi ya
timu zimepangiwa kucheza mechi nyingi nyumbani au ugenini wakati wa kumaliza
Ligi Kuu hasa duru la pili linaloanzia Desemba, 2017 hadi Mei, 2018.
Ikumbukwe tu kwamba ratiba hii
ilipangwa kabla ya uongozi wa Rais Wallace Karia na Kamati nzima ya Utendaji
kuchaguliwa katika wadhifa huo.
“Ninachotaka kusema hapa ni
kwamba, Kamati ya Utendaji iliyoingia madarakani Agosti 12, mwaka huu iliona
upungufu na hivyo kuagizwa ratiba ipangwe upya kwa kuzingatia uwiano wa michezo
ya ugenini na nyumbani ili kwa namna moja au nyingine kusiwe angalau na hisia
za kupanga matokeo,” amesisitiza.
Vita ya upangaji wa matokeo ni
kubwa sana ambayo FIFA wamekuwa wakihubiri na kuagiza mashirikisho katika
mabara yote kadhalika mashirikisho ya nchi kupiga vita upangwaji wa matokeo.
Kidao amezungumza hayo baada ya
kukutana na wanahabari kwa mara ya kwanza tangu kueuliwa kushika wadhifa wa
Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Post a Comment