SDF SPORTS SDF SPORTS Author
Title: WARUNDI WAFIA TAIFA ILA MAVUGO ANA BALAA
Author: SDF SPORTS
Rating 5 of 5 Des:
Simon Msuva akishangilia goli pamoja na Farid Mussa Ushindi wa 2-1 walioupata Taifa Stars leo kwa mabao ya Saimon Msuva na Mbaraka Yusu...
Simon Msuva akishangilia goli pamoja na Farid Mussa

Ushindi wa 2-1 walioupata Taifa Stars leo kwa mabao ya Saimon Msuva na Mbaraka Yusuph kwa upande wa Taifa Stars huku bao la Burundi likipachikwa wavuni na Laudit Mavugo, umehitimisha vyema mechi za kirafiki zilizokuwa katika kalenda ya Fifa kwa upande wa Taifa Stars.

Kama ilivyo ada kwa miaka ya karibuni wakikutana Taifa Stars na Burundi iwe mechi ya kirafiki au kimashindano, nyasi huwa zinawaka moto. Ndivyo ilivyokuwa pia katika mchezo wa leo uliovurumishwa katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam Tanzania. Mchezo ulianza kwa kasi  na kuwachukua Taifa Stars dakika 4 tu kufika langoni kwa Burundi "Intamba Murugamba" kwa shambulizi kali lakini shuti lililopigwa na Farid Mussa liliokolewa  na kipa wa Burundi Nayimana Jonathani.

Burundi hawakuwa wanyonge kwani nao walijibu mashambulizi kwa kushambulia lango la Stars dakika ya 9 na kupata kona ambayo haikuzaa matunda. Mchezo ukiendelea kuwa wa kuvutana huku Stars wakionekana kuwa imara zaidi hasa sehemu ya katikati ya uwanja. Dakika ya 20 Stars walibisha tena hodi kagika lango la Burundi na kufanikiwa kuandika bao la kwanza lililofungwa kwa shuti kali na winga hatari Saimon Msuva baada ya kupokea pasi murua ya kichwa toka kwa Ibrahim Ajibu.

Burundi walibadilika na kuanza kuliandama lango la Taifa Stars  na kufanikiwa kupata kona dakika ya 28 ambayo haikuzaa matunda, dakika ya 30 Burundi walipata pigo huru nje ya 18 lililopigwa na Laudit Mavugo na kutoka nje sentimita chache katika lango la Stars. Hali ya vuta nikuvute iliendelea na dakika ya 35 Saimoni Msuva akiunganisha majalo ya Shomari Kapombe alipiga kichwa dhaifu kilichodakwa na kipa Nayimana Jonathani. Burundi wakajibu mapigo dakika ya 42 Nzeyimana Djuma alikosa bao la wazi akiwa anatazamana yeye na mlinda mlango wa Stars Deogratius Munishi "Dida".

Mpaka filimbi ya mwamuzi Israel Nkongo inapulizwa kuashiria kuwa dakika 45 za kwanza zimemalizika Taifa Stars ilikua mbele kwa bao 1-0.

Baada ya mawaidha, ushauri na maelezo ya mabenchi ya ufundi ya timu zote mbili, kipindi cha pili kilianza kwa kasi ya aina yake na ikawachukua Taifa Stara dakika 2 tu kufika langoni mwa Burundi lakini Ibrahim Ajibu alishindwa kuunganisha vyema krosi ya Mohamed Hussein na kupiga kichwa kilichopaa juu ya lango la Burundi.

Dakika ya 8 ya kipindi cha pili, mpira mrefu toka katika beki ya Burundi ukichagizwa na kutokua makini kwa walinzi wa Taifa Stars ulitua mguuni mwa mshambuliaji wa Burundi anayekipiga katika klabu ya Simba aliyetumia nafasi hiyo kumtazama mlinda mlango wa Stars Dida amekaaje na kufunga goli kwa ustadi mkubwa na kufanya ubao wa matokeo kusomeka 1-1.

Mchezo uliendelea kuwa wakutafutana huku kila timu ikitafuta goli kwa nguvu. Dakika ya 12 kipindi cha pili Mwalimu Mayanga alifanya mabadiliko kwa kumtoa kiungo Salum Abubakary na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Saidi Hamis Ndemla ili kuzidi kuimarisha timu eneo la kiungo. Katika dakika ya 17 kipindi cha pili Taifa Stars walipoteza nafasi ya wazi kabisa mara baada ya kupata mpira wa adhabu ndogo ndani ya 6 ya Burundi baada ya kipa wa Burundi Nahimana Jonathan kudaka mpira aliorejeshewa na beki wake lakini faulu hiyo iliyopigwa na Ajibu haikuzaa matunda.

Hali ya mchezo ilizidi kuwa yenye kashikashi kwa pande zote na kupelekea kosakosa kwa kila upande. Dakika ya 19 kipindi cha pili Farid Musa alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji chipukizi wa Kagera Sugar Mbaraka Abeid.

Burundi walifanya shambulizi kali dakika ya 27 kipindi cha pili baada ya shuti kali lilopigwa na Urasenga Dany kumshinda mlinda mlango Deogratius Munishi  na kugonga mwamba kisha kutolewa na mabeki wa Stars na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda kwa Burundi.

Dakika ya 32 kipindi cha lala salama Mbaraka Abeid ukiwa mchezo wake wa kwanza kuichezea Taifa Stars  kijana huyu aliechukua nafasi ya  Farid Mussa aliiandikia Taifa Stars bao la pili baada ya pasi ya kichwa toka wa Ndemla kumshinda beki wa Burundi na Mbaraka kubaki yeye na mlinda mlango wa Burundi jaribio lake la kwanza kutaka kufunga mpira ulichezwa kidogo na kipa ukagonga mwamba kisha ukamrudia tena Mubaraka Abeid mara hii hakufanya ajizi akaweka kimiani.

Mara hii Burundi walikuja juu lakini ngome ya Stars chini ya Abdi Banda ilikua imara. Ili kuimarisha zaidi na pengine kuuweka ushindi katika mikono salama Mwalimu Mayanga dakika ya 34 alimtoa Mzamiru Yassin na kumuingiza kiungo Jonas Mkude alieenda kuimarisha eneo la kiungo la Taifa Stars.

Dakika ya 41 Ibrahim Ajibu alionekana akichechemea na kufanyiwa matibabu kisha kutolewa nafasi yake ikachukuliwa na Shizza Kichuya, hata hivyo mabadiliko hayo hayakuleta mabadiliko yoyote. Dakika za nyongeza za mwamuzi Israel Nkongo almanusura zitumiwe vizuri na Burundi baada ya mshambuliaji Laudit Mavugo kuwatoka walinzi wa Stars kisha kupiga pasi nzuri iliyomfanya mshambuliaji Urasenga Dany kubaki yeye na mlinda mlango Dida lakini katika hali ya kuwaza afanye nini beki wa Stars waliondosha hatari hii na kuwaacha Burundi wakimlalamikia mwamuzi kuwa ile ni penati lakini mwamuzi Nkongo aliekua karibu kabisa na tukio lile alimzawadia mshambuliaji wa Burundi kadi ya njano kwa kosa la kujiangusha.

Kipyenga cha Israel Nkongo chenye uashirio wa kumalizika mchezo huu kilipulizwa na Taifa Star kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.


Katika mchezo wa leo Burundi walifanya mabadiliko ya kumtoa Ndayishimiye Youssouf nafasi yake akachukua Urasenga Dany, Nzeimana Djuma alitoka akampisha Sabu Mukama na Fataki Ally aliingia kuchukua nafasi ya Nshirimana David.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top