![]() |
Shekhan Rashid wa pili kutoka kulia akiwa katika timu ya taifa |
Shekhan amewahi kuzichezea timu za Moro United, Simba, Mtibwa Sugar, Singida United, Mzizima United, Azam FC na soka la kulipwa nchini Sweden.
Katika mwendelezo wa SDF Sports kuwaletea historia za wachezaji, leo ina mwangazia Shekhan Rashid aliyepata kuwika na timu kadhaa nchini haswa Simba SC.
HISTORIA YAKE YA SOKA
Shekhan historia yake ya soka ilianzia katika timu ya Friends Rangers chini ya Herry Mzozo ambapo ndipo kilipoibuliwa kipaji chake na kuianza rasmi safari ya kisoka. Mwaka 1998 alijiunga na Kilimani FC ya Zanzibar iliyokuwa ikishirikia ligi daraja la pili aliyodumu kwa mwaka mmoja ambapo mwaka 1999 akajiunga na timu ya Mji Mpwapwa ya Dodoma ikiwa ligi daraja la kwanza chini ya kocha Mbwana Makata. Shekhan na wenzake wakaipigania mpaka wakaipandisha ligi kuu. Oktoba 1999 akajiunga na Singida United ambapo pia hakudumu sana kwani mwaka uliofuata baadhi ya watu akiwemo Kassim Dewji waliamua kumpeleka nchini Mauritius kwenye timu ya Association Sportive Port Louis (ASPL 2000). Shekhan alishindwa kucheza ligi ya Mauritius kwa muda wa miezi saba kwasababu ligi yao ilikuwa imefungwa na Serikali kutokana na vurugu zilizokuwa zimetokea kabla ya kuamua kurudi nchini ili kujiunga na timu yake ya Singida United, japo aliporejea aligoma kujiunga nayo.
Wakati timu ya Simba wakiwa wanawafanyia wachezaji majaribio kwenye viwanja vya jangwani kiungo huyo alihudhuria ambapo wachezaji wasiopungua 250 walishiriki. Licha ya lundo hilo la wachezaji waliohudhuria majaribio hayo ya kujiunga na Simba, Shekhan alifanikiwa kupenya na kusajiliwa rasmi na Wekundu hao wa Msimbazi kwa ajili ya msimu wa ligi wa 2001/02.
AINGIA SIMBA KWA KISMATI
Shekhan alisema: "Wakati najiunga na Simba mwaka 2001, Simba ilikuwa imekaa miaka mitano bila kutwaa kombe lolote ila mwaka huo tulishinda vikombe vingi, na tulimaliza ligi kwa kufungwa mechi moja tu na Moro united, chache tukitoka sare na nyingi tukishinda. Furaha yangu kubwa ilikuwa ni kuisaidia timu katoka kwenye ukame wa mataji. Mwaka 2001/ 02 tulishinda kombe la FAT, Kombe la Tusker, ligi kuu bara na kombe la Kagame.
![]() |
Shekhan Rashid (wa kwanza kulia) akiwa katika kikosi cha Simba SC |
MAMA ASHINDWA KUMSHUHUDIA AKICHEZA SIMBA
Shekhan alisema "kucheza kwangu Simba nilikuwa na furaha ila nilikua naumia sana kila nikimkumbuka marehemu Mama yangu. Wakati nikiwa mdogo Mama alikuwa mshabiki mkubwa wa Simba na mimi nilikuwa mtoto wa mwisho kwetu hivyo nilikuwa karibu sana na mama. Mwaka 1996 Mama alifariki kwa hiyo wakati najiunga Simba 2001 na kuichezea kwa mafanikio makubwa Mama hakuniona. Nilitamani sana mama ayaone mafanikio yangu ndani ya Simba ila ndiyo hivyo kazi ya Mungu haina makosa.
SALVATORY EDWARD AMFANYA KUPENDA SOKA
Licha ya kipaji binafsi mara nyingi katika kila fani kuna mtu anakuwa sababu ya wewe kupenda fani fani hiyo, vivyo hivyo Shekhan katika soka alivutiwa na Salvatory Edward mpaka kujikuta amekuwa mchezaji mahiri.
"Nilikua napenda sana kumuangalia Salvatory nilikuwa natamani kucheza kama yeye na nilipata bahati ya kucheza nae timu ya Taifa. Alinisaidia sana pia kunishauri vitu vingi wakati tukiwa timu ya Taifa".
AMKUBALI WAZIRI MAHADHI 'MENDIETA'
"Wakati nikiwa Simba nilikuwa napenda sana kukutana na Waziri Mahadhi 'Mendieta' wa Yanga sababu tulikuwa tunaonyeshana ufundi, na uzuri kila mmoja alikuwa anamkubali sana mwenzie.
KWA SASA AKOSHWA NA NDEMLA, HIMID NA MSUVA
Shekhan anasema akiwa mchezaji alikuwa akimkubali sana Waziri Mahadhi ila kwa sasa wako anawakubali vijana wengi wanaocheza soka nchini ambao ni Said Ndemla, Himid Mao, Saimoni Msuva na Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr'.
AWAONYA WAAMUZI KUELEKEA MWISHO WA MSIMU
Zikiwa zimesalia mechi sita kwa kila timu kumaliza mechi zake za ligi Shekhan amewataka maamuzi kufuata sheria 17 za soka ili bingwa apatikane kihalali bila kuwa na malalamiko.
AWATAKA WATANZANIA WAIUNGE MKONO TAIFA STARS
Shekhan alisema ili kufanikiwa kufanya vizuri kwa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' lazima kuwe na mshikamano wa wadau wote. "Kikubwa ni kuipa sapoti timu yetu ya Taifa, tuache Usimba na Uyanga. Tukifanya hivyo nina imani tutafanya vizuri sababu kuna vijana wengi wenye uwezo".
LIGI YA BONGO NI DHAIFU
Shekhan ametaja moja ya sababu ya klabu za Tanzania kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa kunatokana na udhaifu wa ligi.
"Udhaifu mkubwa upo katika ligi yetu. Ligi haina ushindani imejaa ujanja ujanja mwingi ambao hausaidii lolote inapokuja kwenye mechi za kimataifa. Inatakiwa ligi iwe na ushindani na bingwa apatikane kihalali ndiyo tutaweza kufanya vizuri.
MSHABIKI WA MAN UNITED NA BARCA
Barani Ulaya Shekhan ni shabiki mkubwa wa Manchester United na pia napenda aina ya soka inayochezwa na FC Barcelona. Kwa upande wa wachezaji anamkubali Ronaldinho Gaucho ila kwa sasa navutiwa zaidi na Lionel Messi.
KUHUSU FAMILIA
"Nimeoa tangu mwaka 2010. Tumebahatika kupata watoto watatu, wa kwanza anaitwa Mariam (5), wa pili anaitwa Jamal (4 ) na wa tatu anaitwa Khalif ana miezi miwili.
JAMAL KURITHI MIKOBA YA BABA YAKE
"Wanangu wote wanapenda mpira hasa huyu wa pili Jamal anapenda sana soka. Kama akionyesha kupenda zaidi mpira nitamsapoti kwa asilimia zote ili aje aendeleze nilipoishia mimi.
NJE YA SOKA ANAPENDA MUZIKI NA ANAMKUBALI DIAMOND PLATNUM
"Nje ya soka napenda kusikiliza muziki hasa wa nyumbani. Nikisikiliza kazi za wasanii wa nyumbani nafarijika sana ila nampenda Diamond Platinum. Anautangaza muziki wetu, anapambana, kautoa muziki sehemu moja kaupelekea sehemu nyingine. Saluti sana kwake Diamond Platnumz.
Hiyo ni historia ya Shekhan Rashid Abdallah alipotoka na alikopitia mpaka anastaafu soka la ushindani. Mbali na historia yake kisoka naamini pia nje soka utakua umemjua pia kupitia makala hii.
Post a Comment