Rais wa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Afrika, Issa Hayatou ameteua Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kuwa miongoni mwa wajumbe 11 wa Kamati maalumu ya
mageuzi ya muundo wa CAF itakayokuwa na jukumu la kufanya mabadiliko mapya ya
shirikisho, imefahamika.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAF,
katika Kamati hiyo ikayoongozwa na Rais Issa Hayatou mwenyewe, Malinzi
ameteuliwa katika Kamati hiyo iliyotangazwa leo Oktoba 30, 2016 kutoka ukanda
wa Afrika Mashariki.
Kamati hiyo imeundwa ikiwa ni
sehemu ya maazimio ya mkutano uliopita wa kawaida wa CAF uliofanyika Septemba
29, mwaka huu ambako Rais Hayatou amezingatia mjadala uliolenga kufanya
mabadiliko CAF kwa kufanyia kazi mara moja.
Hayatou si tu kwamba amejali mjadala
wa mkutano ule, pia ameheshimu mawazo ya vyama wanachama vya nchi pamoja na
wajumbe wa Kamati ya Utendaji na wataalamu mbalimbali ili kupata mustakabali wa
muundo wa uongozi wa shirikisho hilo ili kukabiliana na changamoto dhidi ya
mpira wa miguu barani Afrika.
Akizungumzia uteuzi huo, Malinzi
kwanza alimshukuru Hayatou kwa uteuzi huo ambao umeonyesha moja kwa moja kuwa
na imani naye katika kuleta maendeleo ya mpira wa miguu katika muundo mpya.
“Lakini sifa hii ya kuteuliwa ni
yangu pekee kwani ni heshima kubwa ambayo imepewa nchi yetu pendwa ya Tanzania,
kadhalika nchi zote za Afrika Mashariki na Kati,” alisema Malinzi alipozungumza
namtandao wa TFF ambao ni www.tff.or.tz.
Kamati hiyo itawajibika kwa
Kamati ya Utendaji ya CAF ili kupata mwongozo ingawa haibanwi zaidi na Katiba
ya shirikisho.
Kamati inaundwa na:
1. Issa Hayatou (Cameroon), ambaye ni Rais
CAF atakayekuwa Mwenyekiti.
2. Amadou Diakite (Mali), Makamu Rais wa
CAF na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho.
3. Mohammed Raouraoua (Algeria), Mjumbe wa
Kamati ya Utendaji CAF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Masuala ya Sheria. Pia ni
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Algeria (FAF).
4. Lydia Nsekera (Burundi) Mjumbe wa Baraza
la Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
5. Raymond Hack (Afrika Kusini), Mwenyekiti
wa Bodi ya Nidhamu ya CAF.
6. Me. Prosper Abega (Cameroon), Mwenyekiti
wa Bodi ya Rufaa ya CAF.
7. Jamal Malinzi (Tanzania), Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
8. Me. Augustin Senghor (Senegal), Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Senegal (FSF)
9. Victor Adolfo Osorio (Cap Verde), Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Cap Verde (FCF)
10. Maclean Letshwti (Botswana), Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Botswana (BFA)
11.
Hicham El Amrani (Morocco) ambaye ni Katibu Mkuu wa CAF.
Post a Comment