Mchezo wa kwanza wa
mpira wa miguu wa ufukweni, kati ya Tanzania na Ivory Coast unatarajiwa
kufanyika leo kuanzia saa 10.00 jioni kwenye Uwanja uliotengenezwa maalumu kwa
ajili ya mchezo huo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es
Salaam.
Tanzania imepania kufanya
vyema dhidi ya Ivory Coast iliyoingia Dar es Salaam, usiku wa kuamkia Jumanne
kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza wa kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Mataifa
ya Afrika ambako fainali zake zitafanyika Lagos, Nigeria.
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Ali
Sharif ‘Adolph’, licha ya kupania mchezo huo, anakiri anakutana na timu ngumu
ambayo inashika nafasi ya pili barani Afrika, lakini watatumia uzoefu kupata
ushindi ili kuweka historia katika mchezo huo nchini.
Mchezo huo utakaochezeshwa na
waamuzi kutoka Uganda ambao ni Shafic Mugerwa atakayepuliza kipyenga na
wasaidizi wake ni Ivan Bayige Kintu na Muhammad Ssenteza, Mtunza muda atakuwa
Adil Ouchker wa Morocco huku Kamishna akiwa ni Reverien Ndikuriyo wa Burundi.
Timu hizo zinatarajiwa kucheza
mechi mbili za kuwania kufuzu kwani mara baada ya mchezo wa Dar es Salaam,
zitarudiana tena Ivory Coast na mshindi wa jumla atakuwa amefanikiwa kufuzu kwa
fainali.
Kwa upande wa Tanzania, Kocha
Mkuu wa timu hiyo, John Mwansasu, anaendelea na mazoezi na wachezaji wake 16
aliowatangaza wiki iliyopita. Kikosi hicho kinaundwa na wachezaji sita kutoka
Zanzibar na 10 Tanzania Bara.
Wanaounda kikosi hicho ni Talib
Ame, Ahamada, Mohammed Makame, Ahamed Rajab (golikipa) Khamis Said na Yacob
Mohamed wote kutoka Zanzibar. Wengine ni Ally Raby, Mwalimu Akida, Khalifa
Mgaya, Rolland Revocatus, Juma Sultan, Rajab Ghana, Samwel Salonge, Kashiru
Salum, Juma Juma na Kevin Baraka.
Post a Comment