Kocha Mkuu wa timu za vijana Tanzania, Kim Paulsen, amevutiwa
na uwezo wa vijana wanaoibuka kila mwaka katika soka nchini na kusema tuna
hazina ya wachezaji wenye uwezo wa kucheza mahala popote duniani.
Poulsen amewaambia waandishi wa habari leo
Jumanne Septemba 26, 2017 jijini Dar es Salaam kwamba wamefanikiwa kuona uwezo
wa vijana kwa wakati wote, lakini umahiri umekuwa ukiongezeka kwa kila timu
mpya inapoitwa.
Kwa takribani mwezi mmoja,
Kocha Poulsen akishirikiana na Oscar Mirambo walikuwa kwenye programu ya kuinoa
Serengeti Boys mpya.
“Hii Serengeti mpya
inayokuja, nayo ni bora kama ilivyo kwa wale waliopita. Bado naona kuna vipaji
vikubwa sana. Ni kulea tu hawa vijana kazi ambayo tutaendelea nayo.”
Poulsen - Raia wa Denmark
amesema kambi ya vijana 57 walioripoti na kufundishwa na makocha hao,
wameonesha uwezo mkubwa, lakini kiufundi wamepunguza hadi hadi kubaki 27.
Amesema hao waliobaki
watapangiwa kambi nyingine itakayoanza Novemba 19, 2017 na itafikia mwisho
Desemba 19, mwaka huu baada ya kuivunja kambi ya muda jana Septemba 25,
mwaka huu.
Katika programu ya kambi hiyo
mpya ya Novemba na Desemba, Kocha Kim ametaka angalau mechi moja ya kirafiki ya
kimataifa huku akisisitiza apate timu ya nchi iliyowekeza hasa katika soka la
vijana: “Ikiwezekana hata mbili.”
Akizungumzia kuhusu ujio mpya
wa timu ya taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 - Ngorongoro Heroes,
Kocha Kim amesema itaitwa kambini wakati wowote kuanzia Oktoba mwanzoni kwa
kambi ya wiki tatu.
“Timu ya Serengeti Boys
iliyopita ilifanya vizuri sana. Ni matarajio yetu hata hii itafanya vizuri,
lakini hapa nataka nizungumzie ile iliyoshiriki fainali za AFCON u17 nchini
Gabon…
“…kwa hiyo kambi itakayoitwa
ya Ngorongoro Heroes, tutaita wale wote waliounda Serengeti Boys iliyopita.
Hata wale ambao hawakubahatika kwenda Gabon tutawajumuisha kwa ajili ya kambi
ya wiki tatu mwezi Oktoba,” amesema Poulsen.
Amesema kwamba sababu za
kuita nyota wale wa Serengeti Boys katika Ngorongoro Heroes ni kuwapa nafasi ya
kwanza wao kuonekana kama wangali na uwezo wa kupambana kama ilivyokuwa zamani
na kwa wale wenye uwezo tu, ndio watakaochukuliwa,” amesisitiza.
Post a Comment