KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki
na Kati, Azam FC, imefanikiwa kushika usukani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara (VPL) baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 1-0 muda mchache uliopita.
Azam FC inakuwa timu ya tatu kwenye ligi hiyo
ukiachana na Simba na Mtibwa Sugar, kufanikiwa kukaa kileleni mwa msimamo wa
ligi hiyo msimu huu baada ya kufikisha jumla ya pointi saba.
Bao pekee la Azam FC limefungwa na
mshambuliaji Mbaraka Yusuph dakika ya 43 akimalizia pasi ya safi aliyopenyezewa
na Yahya Zayd, aliyewahadaa mabeki wa Kagera Sugar kabla ya kumsetia Yusuph.
Hilo ni bao la kwanza la mashindano la Yusuph
tokea ajiunge na Azam FC, akiifunga timu yake ya zamani aliyoichezea msimu
uliopita kabla ya kutua kwa matajiri hao wa viunga vya Azam Complex msimu huu.
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la
Mapinduzi walifanikiwa kucheza vema kwenye mchezo huo hasa kipindi cha kwanza,
wakionyesha kandanda la kasi huku Yusuph na Zayd wakionekana kuwa kivutio baada
ya kuipa wakati mgumu safu ya ulinzi ya Kagera Sugar.
Kwa ushindi huo, hivi sasa Azam FC imefanikiwa
kuandika rekodi ya kipekee baada ya kucheza mechi tatu za mwanzo za ligi bila
kuruhusu wavu wake kuguswa (cleensheet) ikiwa imefunga mabao mawili tu.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC
kinatarajia kupumzika kwa siku mbili kesho na Jumapili kabla kurejea mazoezi
Jumatatu asubuhi kujiandaa na mtanange ujao dhidi ya Lipuli utakaofanyika
Uwanja wa Azam Complex Jumamosi ijayo Septemba 23 saa 1.00 usiku
Source : Azam website.
Source : Azam website.


Post a Comment