SDF SPORTS SDF SPORTS Author
Title: EMILY MGETA, MTANZANIA ANAYECHEZA SOKA NCHINI UJERUMANI
Author: SDF SPORTS
Rating 5 of 5 Des:
Emily Mgeta akiiwakilisha timu yake katika ligi daraja la tano nchini Ujerumani Emily Mgeta, Mzaliwa wa wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza ...
Emily Mgeta akiiwakilisha timu yake katika ligi
daraja la tano nchini Ujerumani
Emily Mgeta, Mzaliwa wa wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza si jina geni kwa sasa kwa wadau na wanamichezo nchini. SDFsports ilimtafuta Mtanzania huyu anayekipiga nchini Ujerumani katika timu ya Sport Freund Lauffen ya ligi daraja la tano (Verbansliga) na kupiga nae mastori ili Watanzania wapate kumjua alipotokea, alipo sasa na anapotarajia kuwepo siku zijazo.

Mwandishi: Habari yako Emily Mgeta

Mgeta: Nzuri tu, karibu.

Mwandishi: Asante, Watanzania wengi wamekuwa wakisikia tu kuna mchezaji Mtanzania anakipiga nchini Ujerumani, lakini ni dhahiri wengi hawakujui vizuri historia yako wapi ulipotoka, ulipo sasa na malengo yako ya baadae. Kupitia SDFsport hebu waeleze Watanzania historia yako japo kwa ufupi.

Mgeta: Naitwa Emily Mgeta, mzaliwa wa Ukerewe Mkoani mwanza. Historia yangu kisoka inaanzia wilayani Ukerewe ambapo mwaka 2009 nikiwa kidato cha tatu nilichaguliwa ktk timu ya Copa Cocacola ya wilaya na kwenda kushiriki mashindano ya Copa Cocacola mkoa wa Mwanza. Nikapita katika akademi ya Tanzania Street Children Academy (Tsca) ya mkoani Mwanza kuanzia 2009-2010, nikaenda akademi ya Tinsela ya wilayani Magu mkoani Mwanza na kisha nikarejea tena katika akademi TSCA. Baada ya siku chache kurudi TSCA tulisafiri mpaka Arusha kwenda kushiriki michuano ya Rollingstone Cup. Katika michuano ile ya Rollingstone tulitolewa robo fainali na kurudi nyumbani Mwanza. Baada ya kurejea mkoani Mwanza nilipigiwa simu na kiongozi wa Tinsela Bw. Geoffrey Tinsela, akinitaarifu kuwa natakiwa kwenda jijini Dar es Salaam katika mchujo wa timu ya Taifa ya vijana U20 maarufu kama Ngorongoro Heroes. Nawashukuru sana makocha Kim Poulsen na Adolph Rishard ambao waliniamini na kunichagua katika timu ile ya Ngorongoro Heroes na kujumuishwa katika kikosi kilichoshiriki Cosafa ya U20 nchini Botswana ambapo tulitolewa hatua ya robo fainali. Baada ya kutoka Botswana katika michuano ya COSAFA, nikiwa najiandaa kurudi Mwanza nilipigiwa simu na Mutani Yangwe Mkurugenzi wa TSCA  akinijulisha kuwa nisiondoke na badala yake niende nikaonane na kiongozi wa Simba B Patrick Rweyemamu, ili kuzungumza mipango ya mimi kujiunga na Simba B. Baada ya kuonana naye tulikubaliana na bila kuchelewa nilijiunga na Simba B, hiyo ilikuwa ni mwaka 2012.

Mwandishi: Simba B ilikutambulisha zaidi katika tasnia ya kandanda nchini. Ni mafanikio gani uliyoyapata ukiwa Simba B?

Mgeta: Mafanikio niliyoyapata Simba B ni pamoja na kuchukua vikombe vya Kinesi cup na lile la Bank Abc. Pia Simba B ilikuwa njia yangu rahisi kwenda timu ya wakubwa ya Simba.

Mwandishi: Ni jambo lipi limewahi kukufurahisha zaidi ukiwa Simba na lipi limewahi kukuumiza zaidi?

Mgeta: Kitu kilichonifurahisha zaidi Simba B ni kiongozi wetu Patrick Rweyemamu jinsi alivyokuwa akiishi na sisi wachezaji wake na yale maisha ya umoja tuliyokuwa tukiishi wachezaji wa Simba B. Tuliishi kama familia moja kiukweli ilikuwa inanifurahisha sana nayamisi sana. Kingine nilifurahia sana kucheza mechi ya kirafiki ya kwanza ya kimataifa dhidi ya Tusker kutoka nchini Kenya nikiwa katika kikosi cha kwanza. Jambo lililoniumiza sana Simba ni siku niliyosababisha penati katika Mapinduzi Cup dhidi ya Azam fc na kutolewa na Azam katika nusu fainali, sikuweza kulala kabisa kwa maumivu niliyokuwa nayo siku ile.

Mwandishi: Baada ya Simba ulienda timu gani?

Mgeta: Mwaka 2014 nilijiunga na Police Moro niliyodumu nayo kwa muda mfupi na mwaka 2015 nikatimkia huku Ujerumani.

Mwandishi: Nani aliyekuona na kuwa mtu wa kati katika kufanikisha wewe kutoka nchini Tanzania mpaka Ujerumani?

Mgeta: Arnifred Lemle, kwa ushirikiano naye wa karibu ndo aliyeniwezesha mimi kuja huku na kuanza maisha hapa Ujerumani.

Mwandishi: Ilikuwa rahisi kupata timu huko au ilibidi uwe na subira na ustahimilivu wa hali ya juu?

Mgeta: Haikuwa ngumu sana kiukweli mara baada ya kufika Ujerumani nilifanya majaribio katika timu ya Neckarsum Sport Union inayoshiriki ligi daraja la tano (verbandsliga), niliweza kufuzu majaribio yangu na hiyo kuwa timu yangu ya kwanza hapa Ujerumani. Baada ya mkataba wangu kuisha niliweza kujiunga na Sport Freund Luffen ambayo nayo pia inashiriki ligi daraja la tano na ndio ninayoichezea hadi sasa.

Mwandishi: Malengo yako kisoka ni yapi?

Mgeta: Kucheza na kufika level za juu zaidi kama Bundesliga, 2Bundesliga na ligi nyingine kubwa barani Ulaya.
Emily Mgeta akiwa mazoezini katika uwanja wa mazoezi wa timu yake inayoshiriki ligi daraja la tano Ujerumani

Mwandishi: Watanzania wangependa kujua faida na pia changamoto zilizopo katika ligi daraja la tano nchini Ujerumani.

Mgeta: Faida ni nyingi sana, unajifunza uwekezaji na uendeshaji wa soka kwa weledi zaidi, pia huku kuna kutanua akili jinsi ya kujipanga kimaisha baada ya kucheza soka utaishi vipi. Kuweza kufikiria na kujipanga nini utafanya hapo baadae. Changamoto kubwa sana ni ubaguzi wa rangi, ukizingatia mimi mtu mweusi basi wenzetu wanabagua sana watu weusi lakini hainikatishi tamaa, nimejidhatiti vya kutosha kupambana katika hali yoyote ili nifanikiwe, hivyo changamoto hizi nakabiliana nazo vyema tu ili nitimize malengo yangu.

Mwandishi: Tukirejea nyumbani, unadhani ni wakati sahihi wa wewe kuitumikia Timu ya Taifa?

Mgeta: Hilo namuachia kocha wa timu ya Taifa mwenyewe, akinijumuisha katika kikosi chake nitafurahi maana napenda kulitumikia Taifa langu na nitajisikia fahari sana siku akinijumuisha katika kikosi chake. Ila yote kwa yote namuachia kocha kwani ndio mwenye maamuzi ya juu ya nani amuite nani asimuite.

Mwandishi: Unavutiwa zaidi na wachezaji gani wa ligi kuu ya Tanzania na barani Ulaya?

Mgeta: Ligi kuu ya Tanzania navutiwa zaidi na Issa Rashid "Baba Ubaya" wa Mtibwa pia na Mohamed Hussein "Zimbwe jr" wa Simba. Huku barani Ulaya navutiwa zaidi na Philip Lahm wa Bayern na Marcelo wa Real Madrid.

Mwandishi: Nini ushauri wako kwa wachezaji wanaocheza hapa nyumbani Tanzania?

Mgeta: Mimi nashauri wapatapo nafasi za kutoka wazitumie, wasijiulize mara mbilimbili watoke kwa wingi wasiogope changamoto kwani huu ndio wakati wao, ukizingatia vijana wengi wanafanya vizuri sana.

Mwandishi: Naamini unafatilia vizuri ligi kuu ya Tanzania, nini utabiri wako kwa timu inayoweza kuibuka na ubingwa msimu huu??

Mgeta: Kiukweli ligi haitabiriki atabeba nani, maana ukiangalia ilivyo sasa katika timu za juu katika mbio za ubingwa zimeachana pointi chache sana, lakini nafasi kubwa nawapa Simba.

Mwandishi: Kuna stori kuwa unamiliki vituo vya kukuza vipaji jijini Mwanza. Hili uhalisia wake likoje?

Mgeta: Naam, ni kweli kabisa nina vituo viwili vya kukuza vipaji ambavyo ni Viyosa kilichopo wilayani Ukerewe na Mugeta Soccer Academy. Malengo makubwa ya kuanzisha vituo hivyo ni kuvumbua vipaji na kuwasaidia wale wachezaji wadogo ili waweze kutimiza malengo yao.

Mwandishi: Uendeshaji wa akademi hizo unawategemea wadhamini, wafadhili au nguvu zako binafsi?

Mgeta: Napambana mimi kama mimi kwa nguvu zangu binafsi, kinachopatikana nakigawa katika uendeshaji wake. Japo kwa sasa nipo katika mipango ya kusaka wafadhili na wadhamini ili tuweze kuendesha akademi zetu kwa weledi mkubwa zaidi.

Mwandishi: Ukipata nafasi ya kuonana na Rais wa Tff na Mh Waziri wa Michezo ungewashauri nini kifanyike  kwa faida na maendeleo ya soka la Tanzania?

Mgeta: Kikubwa cha kuwashauri ni kuwashauri wadau wengi wa michezo kuwekeza katika soka la vijana yani kuwekeza katika akademi zaidi. Sababu soka la leo halihitaji ujanjaujanja zaidi ya uwekezaji ambao lazima uanzie kwa vijana wadogo kabisa, ambao wakitunzwa na kulelewa vizuri basi baadae  wanakuja kuwa faida kwa Taifa na vilabu vyetu.

Mwandishi: Nje ya soka unapendelea nini?

Mgeta: Napenda sana mchezo wa ngumi, muziki na kupiga dramu.

Mwandishi: Mwanamuziki gani anakukosha zaidi na nyimbo ipi ikipigwa ata usiku wa manane utaamka?

Mgeta: Mwanamuziki anaenikosha zaidi ni Alikiba. Nyimbo ninayoipenda sana ambayo ata usiku wa manane ikipigwa nitaamka ni nyimbo ya Kareem ya Alikiba.

Mwandishi: Tumeongea mengi, lakini eneo hili muhimu hatujagusa. Ni kuhusu suala la mahusiano, umeoa, una mchumba au vyote bado?

Mgeta: Hahahaa naishi na mzazi mwenzangu aitwae Janina na tumejaaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume aitwae Tyler

Mwandishi: Muda wa likizo hua unapendelea kufanya nini?

Mgeta: Mara nyingi likizo huwa nakuwa nyumbani nchini Tanzania jijini Mwanza kuangalia na kusimamia vituo vyangu vya kukuza vipaji vya Viyossa na Mgeta Soccer Academy. Lakini muda mwingine wa kawaida hupenda kucheza mpira na mwanangu Tyler kwa sababu anapenda sana mpira.

Mwandishi: Asante kwa ushirikiano wako Emily Mgeta, nakutakia maisha mema ya kisoka na malengo yako upate kuyatimiza.

Mgeta: Asante sana wasalimie nyumbani huko.

Mwandishi: Salamu zimefika.

Naam huyo ndio Mtanzania Emily Mgeta anayekipiga nchini Ujerumani timu ya daraja la tano (Verbansliga) iitwayo Sport Freund Lauffen. Naamini sasa utakuwa umefahamu vizuri kabisa alipotoka, alipo sasa na matarajio yake ya baadae.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top