Licha yakuahidiwa mamilioni ya shilingi, timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeshindwa kutamba nyumbani baada ya kuendeleza wimbi lake la ‘kunyolewa’ kufuatia kuangukia pua kwa kichapo cha magoli 3-0 kwenye mchezo uliomalizika usiku huu kwenye dimba la Amaan visiwani Zanzibar ikiwa ni mchezo wa awali wa kutafuta kufuzu kushiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani.
Mpira ulianza kwa wachezaji wa timu zote mbili kucheza mpira wa kubutuabutua lakini baada ya dakika kadhaa mpira ulitulia na timu zote kuanza kupanga mashambulizi. Lakini Stars bado wameendelea kuwa na matatizo yaleyale ya kupoteza nafasi zinazopaikana kwa kukosa umakini pindi wanapokuwa kwenye eneo la hatari la timu pinzani.
Kipindi cha kwanza kilimalizika huku Uganda wakiwa mbele kwa goli 1-0 lililofungwa dakika ya 38 na Erisa Sekisambu baada safu ya ulinzi ya Stars kutokuwa na umakini pamoja na golikipa Deogratius Munishi ‘Dida’ kuutema mpira uliomkuta mfungaji na kuukwamisha wavuni kiurahisi kabisa.
Stars ilipata nafasi kadhaa dakika za mapema lakini kutokana na kukosa umakini kwa washambuliaji wa kikosi cha Stars nafasi zote zilizotengenezwa ziliota mbawa. Beki wa kulia Shomari Kapombe alipiga krosi mbili lakini zote ziliishia kwa walinzi wa Uganda. Lakini Amri Kiemba, Abdi Banda na Simon Msuva walipata nafasi za kufunga lakini wote walipoteza nafasi hizo.
Dakika za mwanzo za kipindi cha pili Stars walianza vizuri kwani walicheza mpira wa kasi na kuliandama lango la Uganda lakini bado mambo yaliendelea kuwa magumu. Dakika ya 48 Salim Mbonde almanusura aipatie Stars goli baada ya kuunganisha mpira wa kona uliogonga mtambaa panya na kunyakwa na mlinda mlango wa Uganda.
Dakika ya 57 kocha wa Stars Mart Nooij alifanya mabadiliko kwa kumtoa Amri Kiemba na nafasi yake ikachukuliwa na Said Ndemla huku dakika ya 58 John Bocco ‘Adebayor’ aliingia kuchukua nafasi ya Kelvin Friday.
Dakika ya 63 mambo yaliendelea kuwa mabaya kwa Stars kwani Erisa Sekisambu aliiandikia Uganda goli la pili ambalo lilionekana kumaliza kabisa mipango ya Stars ambao walionekana wakicheza kila mtu kivyake na na sio kitimu. Stars ikaanza kupoteza mipira ovyo na kupoteza umakini, Uganda hawakufanya mashambulizi mengi lakini kila walipofika langoni mwa Stars walikuwa ni mwiba ukilinganisha na mashambulizi yaliyofanywa na Stars.
Dakika saba kabla ya pambano kumalizika, Nooij alimuingiza Rashid Mandawa kuchukua nafasi ya Frank Domayo lakini mabadiliko hayo hayakuisaidia chochote Stars kwani jahazi lake bado liliendelea kuzama.
Dakika ya 88 ndipo ndoto za Tanzania ziliota mbawa baada ya Stars kutandikwa goli la tatu lililofungwa kwa mkwaju wa penati na kufuatia Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kumwangusha mchezaji wa Uganda kwenye eneo la hatari. Farouk Meya aliifungia Uganda penati iliyowahakikishia ‘The Cranes’ ushindi wa ugenini.
Stars itakuwa na kibarua kigumu kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa kwenye uwanja wa Namboole jijini Kampala, Uganda wiki mbili zijazo.
Post a Comment