Jina la Fred Felix Minziro Kataraiya Majeshi 'Baba Isaya' kwa hakika hakuna asiyelijua katika medani ya soka nchini, alikuwa mchezaji wa Yanga akihudumu kama mlinzi wa kushoto aliyesifika kwa kucheza kwa jitihada kubwa.
Sifa nyingine kubwa kwa Minziro ni mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa vijana hao wa Jangwani akiwa mchezaji na baadae kocha.
Kama ilivyo kawaida kwa wachezaji wengi wanapostaafu huamua kuingia kwenye ukocha hata Minziro nae alianza kufundisha soka akiwa kocha msaidizi wa Yanga kisha akawa kocha wa Ruvu JKT kabla haijawa JKT Tanzania katika msimu wa 2015/16.
Alikabidhiwa mikoba ya kuifundisha Singida United ikiwa daraja la kwanza na kufanikiwa kuipandisha ligi kuu lakini baada ya kufanikisha jambo hilo alitupiwa virago na nafasi yake ikachukuliwa na Mholanzi Hans Van Pluijm.
Baada ya kutoka Singida Minziro alikabidhiwa timu nyingine ya ligi daraja la kwanza ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) kama kawaida yake akapambana akaipandisha daraja kucheza ligi kuu msimu ujao wa 2018/19.
Wakati tukijua safari hii Minziro atadumu na KMC ghafla juzi uongozi wa timu hiyo ukamtangaza aliyekuwa kocha wa Mbao FC, Ettiene Ndayiragije kuwa kocha wao mkuu. Kwa maana hiyo wanaachana tena na Minziro aliyewapandisha daraja.
Nimekaa natafakari na kujiuliza maswali mengi hivi Minziro hana uwezo wa kuongoza timu ya ligi kuu? kwanini kila anapopandisha timu anakuja anatolewa? Kama walimuamini kumkabidhi timu aiongoze kwenye vita kubwa ya kupanda daraja kwanini asiaminiwe pia kuongoza timu kwenye ligi kuu?
Nadhani ifike hatua viongozi wa hizi timu waanze kuamini uwezo wa Minziro kwenye kufundisha, kuendelea na zile dhana kwamba kazi yake ni kupandisha timu tu liishe, aaminiwe aongoze timu, tumpe heshima yake huyu mtu.
Lakini pia Ushauri kwa Minziro, ifike hatua awe anaingia mikataba ya kueleweka ambayo itawabana waajiri wake waendelee nae ikiwa ataipandisha timu. Lakini kama yeye mwenyewe anaridhika na hichi anachofanyiwa hapo sawa ila kama haridhiki basi ajiongeze aone namna ya kuwabana waajiri wake.
Katika nchi zilizoendelea kisoka, makocha huwa wanaweka vipengele kwenye mikataba wanayoingia vya kuwalinda na kuwafaidisha.
Mfano timu ikiwa bingwa wa ligi huwa kuna ongezeko la pesa kocha anapata, nadhani ifike hatua minziro awe anatumia washauri au wanasheria anapoingia mikataba hasa na hizi timu zinazomfuata wakati zikiwa madaraja ya chini ili awe anafaidika na kazi kubwa anayoifanya.
Kubaki na sifa kwamba yeye ni mtaalamu wa kupandisha timu daraja huku hakuna cha maana anachopata inatakiwa ifike mwisho.
Asanteni. Ramadhan Kareem.
MINZIRO HAAMINIKI LIGI KUU?
Title: MINZIRO HAAMINIKI LIGI KUU?
Author: SDF SPORTS
Rating 5 of 5 Des:
Author: SDF SPORTS
Rating 5 of 5 Des:
Jina la Fred Felix Minziro Kataraiya Majeshi 'Baba Isaya' kwa hakika hakuna asiyelijua katika medani ya soka nchini, alikuwa mchez...
Post a Comment