KAGERA SUGAR WAIPIGA STOP SIMBA
Timu ya soka Ya Simba SC imeweka rehani matumaini ya kutwaa ubingwa baada ya kuruhu kufungwa magoli 2 kwa 1 na Kagera Sugar katika dimba la Kaitaba Mkoani Kagera.
Simba ndio waliouanza mpira kwa kasi na kulishambulia lango la Kagera na dakika ya kwanza tu Saidi Ndemla alipiga shuti kali akiwa nje ya 18 lakini Juma Kaseja alikua makini na kuupangua mpira ikawa kona ambayo haikuzaa matunda kwa Simba.
Dakika ya 27 Mbaraka Yusuf aliweza kuiandikia Kagera goli la kwanza baada ya kupiga shuti kali akiwa nje ya 18 na kuwaacha mabeki wa Simba pamoja na golikipa wao Daniel Agyei wasijue nini chakufanya.
Baada ya goli hilo Simba waliamka na kufanya mashambulizi mfululizo langoni mwa Kagera lakini mabeki wa Wanankurukumbi walisimama imara kuhakikisha hakuna madhara yoyote yanayotokea golini kwao. Mpaka dakika 45 za kwanza zinamalizika matokeo yalibaki Kagera 1-0 Simba.
Kipindi cha pili vijana wa Msimbazi walikianza kwa kasi lakini uzembe uliofanywa na mabeki ndio ikawa faida kwa Kagera baada ya kupata goli lililofungwa na Edward Christopher baada ya kupokea krosi ya Magoma Seleman.
Simba waliendelea kushambulia bila kukata tamaa na dakika ya 62 Mzamiru Yasin aliipatia Simba goli pekee la kufutia machozi baada ya kumalizia mpira uliotemwa na golikipa wa Kagera Sugar Juma Kaseja, kufuatia shuti la karibu la Juma Luizio aliyeunganisha krosi fupi ya James Kotei.
Mpaka mwamuzi anapuliza filimbi ya kumaliza dakika 90 Kagera 2 Simba 1. Kocha wa Simba aliwatoa Shiza Kichuya, Saidi Ndemla na Ibrahim Ajibu na nafasi zao zikachukuliwa na Mohamed Ibrahim, Juma Luizio na Mwinyi Kazimoto. Kwaupande wa kagera walitoka Japhet Makarai, Christopher Edward na Ame Ally nafasi zao wakaingia Themi Felex, Anthony Matangalu na Ally Ramadhani.
Matokeo mengine katika mechi za ligi zilizochezwa leo. Katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam timu ya African Lyon wameshinda goli 1 kwa 0 dhidi ya Stand United. Huko mkoani Mbeya katika dimba la Sokoine Prisons wakatoka suluhu na Mtibwa Sugar. Na mechi nyingine hii leo ilipigwa katika uwanja wa Majimaji mjini Songea iliwashuhudia Majimaji ya Songea ikiwabugiza Toto African ya Mwanza magoli 3-1.
Post a Comment